Nenda kwa yaliyomo

Tafsiri ya Vishazi na Virai vya Kiingereza kwa Kiswahili

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Vishazi ni vifungu vya maneno vyenye kitenzi na virai ni maneno yasiyo vitenzi au vifungu vya maneno visivyo na kitenzi. Makala hii inafanya kazi ya kupatanisha vile vya Kiingereza na vya Kiswahili ili kuonesha uhusiano kati ya lugha na lugha. Sehemu ya kwanza ya maelezo inatoa ufafanuzi wa maana. Sehemu ya pili ya maelezo inaelekeza jinsi ya kusema (kisawe) kwa ufupi.

Maudhui[hariri | hariri chanzo]

Kishazi cha Kiingereza, declare interest kina maana ya kuweka wazi, kubainisha au kuwaambia wakusikilizao/uwaandikiao kuhusu maslahi yako binafsi juu ya jambo au kitu au mada unayozungumzia. Katika kusema kwa ufupi, tamka: nabainisha maslahi binafsi au naweka wazi maslahi binafsi au nawajulisha kuwa nina maslahi binafsi katika hili na kadhalika.

Bad luck ni kishazi chenye maana ya kinahau. Huelezea kutokea kwa jambo lenye athari mbaya bila kutarajiwa au kudhamiriwa. Kisawe chake ni bahati mbaya.

Be consistent ni kishazi chenye maana ya kuwa thabiti; usie/asie/kisicho - badilikabadilika (kimsimamo, kifikra, kilivyo, n.k.). Visawe vyake ni kuwa na msimamo, baki vilevile, usiwe geugeu.

Challenge ni hali ya kujitokeza kwa jambo jipya na gumu ambalo linahitaji juhudi na maarifa kulitatua. Pia: wito kwa mtu, timu, n.k. ili kujitokeza kwenye pambano la kuamua mshindi. Mfano wa kulingana na maana ya kwanza ni kama, Changamoto Zinazokikabili Kiswahili. Kisawe chake kwa Kiswahili ni changamoto.

Critical thinking ni kufikiri kwa kina kunakoambatana na tafakuri, kujiuliza maswali na kuyatafutia majibu. Pia huhusisha ukosoaji ama kuunga mkono dhana mbalimbali baada ya kujiridhisha. Kisawe chake kwa Kiswahili ni fikra tunduizi.

Delivery report ni hati, ujumbe au arafa inayoonesha kuwa kitu kilichotumwa/safirishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine kimefikishwa. Anayepewa ripoti ni mtumaji. Kisawe chake kwa Kiswahili ni hati/arafa ya uwasilishaji [ufikishaji].

Download a file ni mchakato wa kuchukua nakala ya faili (maandishi, taswira, video, n.k.) kutoka sehemu fulani mtandaoni, kuiingiza na kuihifadhi kwenye kifaa chako (simu, kishikwambi, kompyuta, n.k.). Kishazi kisawe: pakua faili.

Good governance ni kirai kinachotaja utawala upasao wa serikali. Hujumuisha utawala wa sheria, kuwa na mipango sahihi ya kuleta maendeleo, kuimarisha demokrasia, kupinga ufisadi, kusikiliza watu, ushirikishi, ukweli na uwazi, n.k. Kisawe chake cha Kiswahili ni utawala bora.

It is unlucky/unfortunate ni kishazi kinachoelezea kutokea kwa jambo isivyotarajiwa au si la kupendeza au baya na la kushitukiza. Kisawe cha Kiswahili ni si bahati, haikuwa bahati.

Sweet melodies: ni dhana inayohusiana na muziki. Inataja uzuri wa ladha ya muziki kulingana na hisia na vionjo vya moyoni vya msikilizaji. Kisawe chake kwa Kiswahili ni mkong'osio murua/mtamu.

Unleash the dragon kwa maana ya neno kwa neno ni kumfungulia au kumwachia huru mnyama wa kidhahania aitwaye dragoni. Maana ya undani ni kujitokeza na kuweka wazi hisia zilizojificha, kutema nyongo, kufanya jambo pevu baada ya kufikia maamuzi kuwa litafanyika, kudhihirisha kipaji, uwezo, n.k. Kisawe cha Kiswahili ni: Vunja ukimya.

Upload a file ni mchakato wa kuingiza faili la kielekroniki (maandishi, taswira, video, n.k.) kwenye sehemu iliyodhamiriwa mtandaoni. Kishazi kisawe chake cha Kiswahili ni pakia faili.

Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Tafsiri ya Vishazi na Virai vya Kiingereza kwa Kiswahili kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.